MAVUNDE: UTEKELEZAJI WA MIRADI YA UJENZI WA MABWAWA YA UMWAGILIAJI ITACHOCHEA KUKUA KWA SEKTA YA KILIMO
Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Anthony Mavunde amesema utekelezaji wa miradi ya mabwawa unaoendelea nchini hivi sasa utasaidia sana kukuza sekta ya kilimo nchini Tanzania na kuongeza eneo kubwa zaidi linalofanya kilimo cha umwagiliaji.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 12 Novemba, 2022 wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa bwawa la Membe linalojengwa Wilayani Chamwino, Dodoma.
"Katika bajeti ya mwaka 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Umwagiliaji imepanga kujenga jumla ya mabwawa 14 nchi nzima, likiwemo bwawa hili la Membe litakalo kuwa na uwezo wa kuhifadhi maji lita Bilioni 12.
Pamoja na bwawa hili kutumika katika shughuli za umwagiliaji, pia litawekwa miundombinu ya kusaidia unyweshaji maji mifugo, kupeleka maji ya matumizi ya majumbani kwa vijiji vinavyozunguka na kuwa sehemu ya utalii kwa wananchi mbalimbali, hatua ambayo itaongeza mapato ya Halmashauri ya Chamwino.
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametuongezea bajeti Wizara ya Kilimo ambapo fedha nyingi zimeelekezwa katika miradi ya umwagiliaji ili kuhakikisha tunakuwa na vyanzo vya uhakika vya maji na kuwezesha wakulima kufanya kilimo zaidi ya mara moja ndani ya mwaka”Alisema Mavunde
Vilevile, Mhe Mavunde alimpongeza Bw. Raymond Mndolwa, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kazi nzuri anayoifanyia ya usimamizi madhubuti wa mkakati wa Serikali wa kendeleza kilimi cha umwagiliaji, na kubainisha kuwa ni wazi kuwa ndoto ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kufikia eneo la umwagiliaji la hekta 1,200,000 ifikapo 2025 linaenda kufikiwa.
Naye Diwani wa Kata ya Membe Wilayani Chamwino, Mheshimiwa Simon Petro Machengu alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea mradi huo mkubwa kwenye Kata yake, na kubainisha kuwa wananchi wa Membe hawana cha kumlipa zaidi ya kumwombea kwa Mungu ili azidi kumpa afya njema na utashi wa kuwatumikia watanzania.
Maoni
Chapisha Maoni