RIWAYA YA ENTANGLEMENTS YAIBUA MJADALA KUHUSU MABADILIKO YA JAMII
Riwaya mpya ya Kiingereza iitwayo Entanglements, iliyoandikwa na Julius John Lwenje, imezinduliwa ikiwa na dhamira ya kuichochea jamii kutafakari mabadiliko yanayotokea katika maisha ya kila siku, hususan katika mahusiano ya kijamii, maadili, changamoto za maisha na mwingiliano baina ya watu katika nyakati tofauti. Kupitia hadithi yenye wahusika na matukio yanayovutia, riwaya hiyo inaangazia namna mabadiliko ya kijamii yanavyoathiri mienendo ya watu, mitazamo yao na uhusiano wao, huku ikiibua maswali kuhusu mwelekeo na mustakabali wa jamii katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi. Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kitabu hicho, mwandishi Julius John Lwenje alisema kuwa riwaya hiyo ni matokeo ya tafakuri yake ya muda mrefu kuhusu maisha na mabadiliko yanayoendelea ndani ya jamii. Alisema kuwa pamoja na kutoa burudani kwa wasomaji, kitabu hicho kinalenga kuelimisha na kuchochea mijadala yenye tija kuhusu masuala mbalimbali yanayoigusa jamii, kwa kuwapa wasomaji fursa ya kutafaka...