Wananchi wa Puma wakishuhudia ukaguzi wa mradi huo.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Singida, Denis Nyiraha akizungumza wakati wa ukaguzi wa ujenzi wa vyoo vya Zahanati ya Puma. Kushoto ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi, Mika Likapakapa na kulia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Kilimba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) Mkoa wa Singida, Yohana Msita, akichangia jambo kwenye ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa vyoo vya Zahanati ya Puma. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa Singida, Dkt.Binilith Mahenge.
Ukaguzi wa madarasa Shule ya Sekondari Ikungi ukiendelea.
Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida imekagua miradi ya maendeleo wilayani Ikungi na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo hususani eneo la maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika chini ya Serikali ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya afya.
Pia kupitia ukaguzi wa utekelezaji wa miradi hiyo CCM kwa namna ya kipekee imeguswa na mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Issuna iliyopo Wilaya ya Ikungi ambao unakwenda kutatua changamoto za wananchi wa eneo hilo za kusafiri umbali mrefu kwenda kata zingine kufuata huduma za afya.
Akizungumza jana wakati wa ziara ya ukaguzi wa utekelezaji wa maagizo ya ilani ya CCM, Mwenyekiti wa kamati hiyo Alhaji Juma Kilimba alihimiza sekta hiyo na nyingine kuhakikisha inakamilisha miradi yote kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.
"Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo nchini kote hivyo nawaomba wasimamizi wa ujenzi wa miradi hii kuwa wazalendo katika matumizi ya fedha hizo,". alisema Kilimba.
Katika hilo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Gutete Mahava akitoa taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo alisema mradi huo ulibuniwa mwaka 2014 na upo Kijiji cha Issuna 'A'
Alisema zahanati hiyo ikikamilika itatoa huduma kwa wananchi wa vijiji vitano vya Issuna 'A, Issuna 'B', Ng'ongosoro, Nkuhi na Tumaini na kuwa ujenzi wake upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Mahava alisema kuwa walipokea Sh.50 Milioni kutoka Serikali kuu na ununuzi wa vifaa vyote umefanyika na tayari Wizara ya Fedha imetenga Sh.8 Milioni kwa ajili ya dawa na vitendanishi.
Hata hivyo kamati hiyo imeomba hatua za haraka zichukuliwe ili kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya wilaya hiyo ambao bado mradi wake unasuasua kutokana na changamoto za kifedha -kutokana na umuhimu wake mkubwa kwa idadi kubwa ya watu wanaozunguka wilaya hiyo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt.Binilith Mahenge akizungumza baada ya kukamilika kwa ziara hiyo aliwashukuru wakurugenzi na wakuu wote wa wilaya zote kwa kusimamia miradi hiyo.
"Niwashukuru wakurugenzi wote na wakuu wa wilaya kwa umoja wenu na kusimamia miradi hii ambayo inatumia fedha nyingi kutoka Serikalini,". alisema Mahenge.
Akizungumzia mradi wa maji wa Kipumbuiko Dkt. Mahenge aliwata wahusika kutoangalia faida zaidi badala yake wazingatie utoaji wa huduma kwa wananchi na kuutunza.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro aliishukuru kamati hiyo na akatumia nafasi hiyo kuelezea mikakati ya maendeleo ya wilaya hiyo hususani katika sekta ya kilimo hasa cha zao alizeti na mpunga ambao unalimwa kwa wingi maeneo ya Iyumbu.
Alitaja eneo lingine watakalo liangalia ili kupata mapato ni kwenye madini, ufugaji wa nyuki na miradi mingine.
Kamati hiyo katika wilaya hiyo ilikagua mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na ofisi moja Shule ya Sekondari Ikungi, ujenzi wa madarasa mawili Shule ya Msingi Ikungi, ukamilishaji wa ujenzi wa Hospitali ya wilaya hiyo, ujenzi wa mradi wa maji Kipumbuiko, ujenzi wa matundu saba ya vyoo Zahanati ya Puma, ufugaji wa nyuki (Kikundi cha Save The Bee Issuna, ukamilishaji wa ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Issuna, ujenzi wa Chuo cha Ufundi cha VETA na ukamilishaji wa ujenzi wa maabara Shule ya Sekondari Ikungi.
Maoni
Chapisha Maoni