TANZANIA KUNUFAIKA NA BILIONI 120/- KUTOKA GEF KULINDA MAZINGIRA
Wadau na Wataalamu wa Mazingira wakiwa katika Warsha inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF jijini Dodoma Februari 13, 2023. |
TANZANIA KUNUFAIKA NA BILIONI 120/- KUTOKA GEF
Tanzania inatarajia kunufaika na mradi wenye thamani ya Shilingi 120 Bilioni kwa ajili ya miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kutoka Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF).
Hayo yamesemwa leo Jumatatu (Februari 13, 2023) Jijini Dodoma na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga wakati akifungua Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF.
Bi. Maganga amewashukuru washirika hao wa maendeleo kwa kuandaa mpango huo wa utoaji wa fedha hizo ambazo hadi sasa tayari zimekwishatolewa katika amwamu na kusema kuwa zitasaidia katika juhudi za kuimarisha uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Aidha Bi. Maganga amewataka wadau na wataalamu hao kutumia vyema ujuzi na uzoefu walionao katika kuimarisha mapambano na changamoto za mazingira zilizopo kwa lengo la kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa miradi chini ya GEF- awamu ya nane inatekelezwa kwa wakati.
“Tanzania ni nchi mnufaika wa miradi ya GEF ambayo inafadhiliwa kupitia mikataba mbalimbali ya kimataifa, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais imeona umuhimu wa kuita wadau na wataalamu kutoka wizara na taasisi za kisekta kutoka mashirika mbalimbali ili kuweka mikakati ya pamoja na kufanikisha ajenda ya mazingira,” alisema.
Aidha, Katibu Mkuu Maganga ametoa wito kwa wataalamu hao kuhakikisha wanafanya maandalizi ya haraka ya kuainisha maeneo ya kipaumbele ya miradi ya washirika wa maendeleo ili kuanza katika uliowekwa na kuikamilisha kwa wakati.
Kwa upande wake Mratibu wa GEF – Kanda ya Afrika Bw. Ibrahima Sow alisema kuwa Tanzania imetengewa mgao huo wa fedha za mzungumzo wa nane katika maeneo matatu ya mradi kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni mradi wa usimamizi katika Maziwa Makuu na Mabonde ya Maji, fedha za kujenga uwezo kwa wataalamu wa miradi pamoja na usimamizi wa miradi katika nchi zinazoendelea.
Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba alisema kuwa katika eneo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhimiza na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.
Alisema kuwa mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa matokeo ya kuongezeka kwa gesijoto duniani sambamba na uharibifu wa uoto asili na bioanuai, hivyo Serikali imeanzisha kampeni za upandaji miti ili kuhakikisha nchi inakabiliana na athari hizo.
Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wadau wa Mazingira Nchini Bw. Tumaini Marijani aliipongeza Serikali kwa namna inavyoratibu masuala ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira nchini.
Tumaini, pamoja na kuhamisha wadau wakiwemo taasisi binafsi kushiriki shughuli za mazingira, pia aliwataka watalaamu na wadau hao kushiriki zoezi la upandaji wa miti ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira.
Warsha hiyo inatoa fursa kwa Tanzania na wadau wa ndani na nje ya nchi kujadili na kupeana uzoefu katika mafanikio na namna ya kutatua changamoto zilizopo na zinazoweza kutokea katika miradi iliyopita na inayoendelea kutekelezwa.
Maoni
Chapisha Maoni