Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba akipokea vitabu vya miongozo na vitabu mbalimbali kutoka kwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi mara baada ya kufanya mazungumzo na Menejimenti ya Mahakama akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam, Leo tarehe 23 Disemba 2020.
Na Mathias Canal, Wizara ya Katiba na Sheria-Dar es salaam
Serikali imeipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kazi kubwa yenye weledi uliotukuka inayoifanya kwa ajili ya kuwasaidia wananchi
Pamoja na pongezi hizo kadhalika mahakama imetakiwa kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa haraka mipango inayojiwekea kwani kutofanya hivyo husababisha utekelezaji wake kuwa wa gharama kubwa pasina sababu za msingi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa rai hiyo tarehe 23 Disemba 2020 wakati akizungumza na Menejimenti ya Mahakama akiwa katika siku ya tatu ya ziara ya kikazi Jijini Dar es salaam.
Dkt Nchemba amesema kuwa serikali itazifanyia kazi changamoto zote zinazoikabili Mahakama kote nchini ili kuhakikisha kuwa wananchi wanahudumiwa ipasavyo ikiwemo mashauri kufanyiwa kazi kwa haraka.
Ameongeza kuwa kunapokuwa na uwezekano wa kutatua mambo kwa haraka ni vyema mahakama na taaisisi zote za serikali kuzitatua bila kuwa na mkwamo wowote ili kuwarahisishia wananchi upatikanaji wa huduma.
Dkt Nchemba amesisitiza kuwa Mahakama pamoja na watendaji wote wa serikali wanapaswa kufanya kazi kwa uthubutu na kuchukua hatua kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza kufanya maamuzi mbalimbali pasina kufanya uonevu kwa wananchi.
Kuhusu kubadilisha sheria, Mwenendo wa mashauri na Hukumu, Amesisitiza maelekezo yake aliyoyatoa wakati alipotembelea Taasisi ya mafunzo ya uanasheria kwa vitendo Tanzania (Law School) kuhusu kubadilisha sheria, Mwenendo wa mashauri pamoja na Hukumu kuwa katika lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe Geofrey Mizengo Pinda ameipongeza mahakama kwa kazi kubwa ambayo inazifanya kuhakikisha wananchi wanapata haki pasina uonevu.
“Kesi nyingi hazijaamuriwa kutokana na vyombo vingi kuingia katika kukamilisha kazi zao ikiwemo Polisi, hivyo kuna kila sababu ya ukamilishaji wa taarifa muhimu za upelelezi ili mahakama iweze kukamilisha utoaji hukumu kwa haraka” Amesisitiza Mhe Pinda
Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Jaji Prof. Ibrahim Khamis Juma, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi ameshukuru kwa ushirikiano inaoupata kutoka Wizara ya Katiba na Sheria kwani bila uongozi madhubuti huenda baadhi ya mambo yangekuwa hayajakamilika.
Jaji Dt Feleshi amesema kuwa ushirikiano huo umeongeza uwajibikaji na utekelezaji wa haraka wa majukumu yake.
MWISHO
Maoni
Chapisha Maoni